Binti atupwa jela mwaka mmoja kwa kosa la KUMBAMBIKIA mtoto mwanaume ili apate fedha ya matumizi
MAHAKAMA
ya Mwanzo Old Shinyanga katika Manispaa ya Shinyanga, imemhukumu Pendo
Joachim (33) mkazi wa kijiji hicho, kutumikia kifungo cha nje cha mwaka
mmoja na kutakiwa kulipa faini ya Sh milioni moja.
Amepewa adhabu hiyo baada ya kupatikana na kosa la kusingizia mtoto kwa mwanamume mwingine ili apate pesa za matumizi.
Akisoma
hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama hiyo, Christian Chovenye alisema
Mahakama imemtia hatiani mwanamke huyo kwa kosa la udanganyifu, ambapo
Deus Njile alikuwa akimhudumia mtoto huyo kwa miaka mitatu mfululizo,
akijua kuwa mtoto ni wake.
Katika
maelezo yake, Njile alidai kuwa alibaini kuwa mtoto huyo si wake, baada
ya kuona kadi mbili za kliniki, zenye majina tofauti ya baba.
Baada ya kubaini hali hiyo, aliamua kwenda kwenye uongozi wa kijiji ili apate suluhu juu ya mtoto huyo.
Ilidaiwa
kuwa mbele ya Uongozi wa Kijiji, mwanamke huyo alikiri kuwa mtoto ni wa
mwanamume mwingine na alifanya hivyo ili apate huduma ya mtoto.
Hata
hivyo, Njile hakuishia hapo bali alipofungua kesi katika Mahakama ya
Mwanzo ya Old Shinyanga, kwa madai ya kusingiziwa mtoto na kumhudumia
kwa miaka mitatu. Njile alitaka Mahakama iamuru alipwe fidia ya fedha,
alizomhudumia mtoto huyo.
Kesi hiyo ilifunguliwa Machi 9, mwaka huu na hukumu ilitolewa Aprili 30, mwaka huu.
Mshitakiwa
alipotakiwa kujitetea, aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa sababu
ana watoto wawili, wanaomtegemea. Pia, alidai yeye ni mgonjwa wa
shinikizo la damu.
Mahakama ilimtaka alipe fedha hizo, Sh milioni moja ndani ya miezi kumi na mbili.
0 comments: