Pata Habari kwa kuandika email yako hapa chini:

RAIS KIKWETE AAGIZA UCHOCHORO WA KUPITISHA MADAWA YA KULEVYA VIWANJA VYA NDEGE UZIBWE HARAKA!



 Rais Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa akizungumza leo, Alhamisi, Aprili 24, 2014, kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Awamu ya Tatu ya Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere wa Dar es Salaam kwenye eneo la Uwanja huo, Kipawa.
 Rais Kikwete akipeana mikono na Balozi wa Uholanzi nchini Mhe Jaap Frederiks baada ya  kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Awamu ya Tatu ya Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere wa Dar es Salaam kwenye eneo la Uwanja huo.
 Rais Kikwete akipata maelezo ya ujenzi wa Awamu ya Tatu ya Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere wa Dar es Salaam kwenye eneo la Uwanja huo.
 Rais Kikwete akieleza jambo baada ya kupata maelezo ya ujenzi wa Awamu ya Tatu ya Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere wa Dar es Salaam kwenye eneo la Uwanja huo.
Rais Jakaya Kikwete akikata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa kuanza ujenzi wa jengo la tatu la la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam leo. Kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba , Balozi wa Uholanzi nchini, Jaap Frederiks, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Injinia Suleiman Suleiman, na Mwenyekiti wa Kamatim ya Bunge ya Uchukuzi Mhe. Peter Serukamba. Kwa picha zaidi BOFYA HAPA
---------------------------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameiamuru Wizara ya Uchukuzi na taasisi zake kuchukua hatua za mara moja kukomesha aibu ya viwanja vya ndege vya Tanzania kutumika katika uchochoro wa kupitisha na kusafirisha madawa ya kulevya.
 
Aidha, Rais Kikwete amesema ukweli kuwa madawa ya kulevya yanazidi kupita katika viwanja vya ndege za Julius Nyerere International Airport (JNIA) na ule wa Kilimanjaro International Airport (KIA) unazidi kuchafua heshima na jina la Tanzania.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza leo, Alhamisi, Aprili 24, 2014, kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Awamu ya Tatu ya Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere wa Dar es Salaam kwenye eneo la Uwanja huo.
Rais ameweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Uwanja huo muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye Ujenzi wa Hospitali ya Kisasa ya Kufundishia na Kutoa Huduma katika eneo la Mlongazila, eneo la Kibamba, Dar Es Salaam. Shughuli zote mbili ni sehemu ya kuadhimisha Miaka 50 ya Muungano.
“Siridhishwi na hali ya usalama katika viwanja hivi viwili na matukio ya kusikia madawa yametokea Tanzania kupitia viwanja vyake na yamekamatwa huko Australia yanachafua sana jina la nchi yetu. Badala ya kuchukua hatua kukomesha jambo hili tunakwenda mbele, tunakwenda nyuma…mbele, nyuma.  Hili haliwezi kuruhusiwa kuendelea. Ni jambo la kutia simanzi sana,” amesema Rais Kikwete na kuendelea:
“Mmeyasema wenyewe…leo kiwanja hiki kinapitisha abiria milioni 2.5 kwa mwaka, mkifikisha abiria milioni sita si mtakuwa soko huria kabisa…..mara leo mwanamuziki huyu kakamatwa Afrika Kusini…mara kesho yule….limalizeni hili haraka.  Nataka tuongeze usalama sana katika viwanja hivi viwili…. vimekuwa kama uchochoro.”
Rais Kikwete amemtaka Waziri wa Uchukuzi  kumjulisha ni maofisa gani wa Idara za Serikali wanahusika kupitisha madawa hayo kwenye viwanja hivyo: 
  “Kama kuna maofisa wa ushuru, ama maofisa wa uhamiaji, ama maofisa wa polisi ama maofisa wa uwanja wa ndege ambao wanashiriki katika mchezo huu wa kupitisha madawa haya nipeni orodha yao,  nitawaondoa kazini. Tusifanye masihara na hili, linatuaibisha sote. Tusiwaonee aibu watu katika jambo hili.”

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
 24 Aprili, 2014

0 comments: